MAANA YA HIP HOP
==>Mahali ilipozaliwa?
Julai 23 mwaka 2007, Jiji la New York,
lilitangaza rasmi kuitambua 1520 sedgwick Ave
iliyoko Bronx kuwa sehemu ambayo hip hop
ilizaliwa. “1520 sedgwick Avenue ni sehemu
ambayo Recreation Room, chumba
alichokitumia muasisi wa hip hop, Dj Cool Herc.
Taarifa ilisema “ingawa kwa sasa (wakati huo
mwaka 2007) umefungwa kwa marekebisho
tangu mwaka uliopita, tunawataka wana hip
hop na wawezeshaji wengine kutoa zabuni ya
kupata uendeshaji wa sehemu hii. Leo hii
waratibu watafanya mkutano wa waandishi wa
habari katika eneo la kihistoria kutangaza kuwa
Jimbo la New York kupitia ofisi ya kuhifadhi
makumbusho na utunzaji wa historia
wameyakubali maombi yaliyotumwa Julai 2
kuitambua rasmi sehemu hii”.
Dj Kool Herc
Ambaye ni mmoja kati ya waasisi wa Hip Hop
anasema “sehemu nilipoanza kupiga muziki
ilikuwa ni 1520 Sedgwick Avenue, katika
recreation room, chumba kilichokuwepo katika
jengo lilipokuwa pango langu, watu walikuja
kucheza muziki kutoka maeneo jirani”
Krs One
Anasema “.mwaka 1973, nilikuwa Bronx, katika
hii sehemu iliyoitwa 1520 sedgwick Ave, hii
ndiyo sehemu ambayo hip hop ilipozaliwa. Mtu
anayeitwa Cool Dj Herc alikuwa akifanya
maenesho..”
Tarehe ya kuzaliwa
August 11, 1973, ndiyo tarehe ambayo hip hop
ilizaliwa kwa mujibu wa Cindy Campbell
ambaye ni dada yake na Dj Kool Herc. Onesho
la kwanza la hip hop lilifanyika siku hiyo.
Onesho hilo liliandaliwa na Dj Kool Herc kwa
lengo la kuchangisha pesa ili dada yake (Cindy
Campbell) aweze kurudi shule (back to school
party). Herc alikodisha recreation room kwa
dola ishirini na tano za kimarekani na kiingilio
ilikuwa ni thumni (cent) 25 kwa wanawake na
thumni 50 kwa wanaume. Herc alikuwa kwenye
mashine na msema chochote (mc) wa siku hiyo
alikuwa ni dada yake (cindy), tukio hili ndilo
linalomfanya cindy Campbell kuwa mwanamke
wa kwanza katika hip hop (first lady of hip
hop).
Charlie Ahearn
Ni mtu ambaye aliyeandaa filamu ya Hip Hop
iitwayo “Wild Style” kuanzia mwaka 1980
mpaka 1982 ilipotoka. Anasema “August 11,
1973 imeibadilisha dunia, tunatakiwa
kusherekea ubunifu na maajabu ya usiku huo”
Licha ya tarehe hiyo Universal Zulu Nation
kupitia tovuti yao wanaitambua tarehe 12 Nov
1973 kama tarehe rasmi ya kuzaliwa hip hop na
pia mwezi November kama mwezi rasmi wa hip
hop. Wanasema “ kwa kuzingatia tarehe tajwa
hakuna kitakachokuwa na umuhimu kama
kusherehekea utamaduni wa hip hop na historia
yake katika mwezi novemba, hakika ndiyo kitu
kilichotufanya Universal Zulu Nation tuwepo
kwa zaidi ya miaka ishirini na saba (kwa wakati
huo)”
WATU NA VYANZO MBALIMBALI
VILIVYOWAHI
KUFAFANUA HIPHOP
Baadhi ya watu na vyanzo mbalimbali vya
habari vimewahi kufafanua Hip Hop kwa nyakati
tofauti tofauti kulingana na mapokeo.
Wafuatao/vifuatavyo ni vyanzo na watu
mbalimbali waliowahi kufafanua maana ya hip
hop:-
AFRICA BAMBATAA
“Hip hop ni harakati za utamaduni mzima.
Unapoongelea kughani (rap), kughani ni sehemu
ya utamaduni wa hip hop. Ughanaji (emceeing),
umanju (deejaying), uvaaji, lugha vyote hivi ni
sehemu ya utamaduni. Wavunjaji (break dance),
namna unavyotenda, unavyokwenda,
unavyotazama (mambo) ni sehemu ya
utamaduni na muziki wake hauna ubaguzi
rangi. Muziki wa hip hop umetokana na weusi,
udhulungi, njano, nyekundu, nyeupe……. ni
sehemu za hip hop”.
DJ KOOL HERC
“Hip hop ni kemia (chemistry) ambayo imetoka
Jamaika.. nilizaliwa Jamaika na nilikuwa
nasikiliza muziki wa kiamerika nikiwa huko
huko. Msanii niliyekuwa nikimpenda ni James
Brown. Ndiye aliyenivutia mimi, nilikuwa
nikicheza vibao vingi vya James Brown.
Nilipokuja hapa (Bronx) nilijiweka katika mtindo
wa kiamerika ili kuendana na mazingira.
Niliweza kukata midundo na kuicheza kwa
muda mrefu na watu wakaipenda, niliwapa
ladha waliyoipenda……’’
DAVEY D
“Hip hop ni utamaduni ambamo ughanaji (rap)
ndimo umeasisiwa. Mwanzoni ulikuwa na nguzo
nne ambazo ni sanaa ya machata (graffiti art),
mavunjanji (break dancing), umanju (dj) na
emceeing (ughanaji). Hip hop ni mtindo wa
maisha ambao una lugha yake, mtindo wa
kuvaa, muziki wake na fikra zake hukua kila
siku. Siku hizi machata pamoja mavunjaji
havitiliwi maanani sana ndio maana neno “rap”
na “hip hop” yanatumika kwa pamoja
kumaanisha kitu kimoja lakini ikumbukwe kila
nguzo zina umuhimu na zinaendelea kuwepo
katika utamaduni”
Anaendelea kusema “tatizo ni kuelewa maana
ya hip hop, mara nyingi huwa inatolewa na
wazungu (whites) wenye vyombo vya habari au
wale ambao huwa wanapata nafasi ya kuhojiwa
katika vyombo hivyo. Huwa wanaelezea maana
ya hip hop kwa manufaa yao na sio kwa
manufaa ya uma na wale waliouasisi utamaduni
huu wa hip hop”
COMMON
“Hip hop ni njia yetu ya kujieleza (expression).
Niliipenda mapema zaidi pindi tu
ilipotambulishwa (hip hop) kwangu. Nilisikia
“the message” ya Melle Mel… nilipenda namna
alivyowasilisha na nilipenda pia alichokuwa
akikisema
SAMIA X
Samia X ni mmoja kati ya waasisi na
waanzilishi wa kundi la KWANZA UNITY
amewahi kusema
“ Hip Hop ni sayansi ya upangaji vina katika
midundo kuelezea maisha yanavyoendelea
katika jamii, Maisha….. ni msigishano na
mpambano unaoendelea kati ya miundo miwili
tofauti kutafuta uwiano sahihi kama giza na
mwanga, starehe na shida,
protini na wanga, majani na miiba ”.
Maneno hayo aliyatoa wakati akifanya
utangulizi katika santuri ya “vina mwanzo, kati
na mwisho” ya mwanamuziki Farid Kubanda
maarufu kama Fid Q.
WIKIPEDIA
Katika mtandao huu, Hip Hop imeelezewa kama
mfumo wa kuwasilisha mawazo kwa kutumia
sanaa ya muziki ambao utamaduni wake
umeasisiwa kutoka katika jamii za wamarekani
weusi na walatino katika miaka ya 1970 jijini
New York hususani katika South Bronx. Kwa
mujibu wa mtandao huu, Hip Hop
imeorodheshewa misingi mitano ambayo ni
Ughanaji(mceeng), mavunjaji (break dancing),
machata (graffiti) ambayo imenukuliwa toka
kwa Afrika Bambaataa. Msingi wa tano
unatajwa kuwa ni Mdundo kinywa (beat
boxing).
WISEGEEK
Tovuti hii inaelezea Hip Hop ni harakati za
utamaduni ambao mara nyingi huwa katika
mfumo wa muziki. Utamaduni huu ulianzia
Bronx katika jiji la New York katika miaka ya
1970. Utamaduni huu ulianza katika jumuiya za
wamarekani weusi ukapewa mchango mkubwa
na jamii za walatino katika ukuaji wake.
Utamaduni wa Hip Hop ulianza kama mtindo
wa maisha uliokuwa handakini kabla ya kuibuka
na kuwa moja kati ya mikondo mikuu ya
maisha duniani. Mfumo huu umejipatia
umaarufu mkubwa kwa kuwa umekua
ukifanywa kibiashara hususani katika taifa la
marekani. Hip Hop inaelezewa kama ni aina ya
muziki ambayo inayohusisha vitu vingi katika
uwasilishwaji wake lakini mara nyingi
huwahusisha zaidi manju na mghanaji.
Katika tovuti hii imetaja nguzo za Hip Hop ni
Djing, Emceeing, break dancing na sanaa ya
Graffiti. Inaelezewa pia wakati mwingine Hip
Hop Fashion, mdundo kinywa (beat boxing), Hip
Hop Slang, Street Knowledge na Street
Enterpreneurship zimekua zikiongezwa kama
nguzo ya tano.
Kwa ujumla
Naweza kusema, “Hip Hop ni utamaduni ambao
huegemea katika kuwianisha kwa usahihi
mambo kwa kutumia zaidi kanuni za kisanaa
kurahisisha milinganyo halisi inayoikumba jamii
husika kwa kutoa taarifa, maarifa na njia katika
kusaidia harakati za ukombozi wa tabaka fulani
linalogandamizwa”.
Muasisi wa utamaduni huu anafahamika kama
Clive Campbell au kwa jina maarufu kama Dj
Kool Herc. Alikuwa ni manju(dj) mwenye asili
ya Kijamaika aliyehamia nchini marekani katika
Bronx mwishoni mwa miaka ya 1960. Asili ya
utamaduni huu wa Hip Hop, unatoka kwa vijana
weusi wa kimarekani pamoja na walatino
walioishi Bronx katika miaka ya 1970. Kwa
wengi unatambulika kuwa unatokana na
wamarekani weusi kutokana na mchango
mkubwa walioutoa katika jitihada za kuikuza
hip hop. Licha ya kuanzishwa na watu weusi
utamaduni huu wa Hip Hop unaweza kufanywa
na mtu yeyote yule bila kujali itikadi za kidini,
kikabila, rangi, lugha au utaifa wa mtu.
Jina la Hip Hop lilikuja miaka michache
baadaye utamaduni huu ulipokomaa na kuwa
mtindo rasmi wa maisha. Katika miaka ya
sabini utamaduni huu uliweza kupata
kufafanuliwa nguzo zake nne za mwanzo kabla
ya tano kuongezeka. Kwa mara ya kwanza
ziliorodheshwa na Afrika Bambaataa. Nguzo
hizo zilikuwa ni Uchenguaji/ughanaji (mceing),
Umanju(deejaying), mavunjanji (break dance)
na machata (graffiti).
Maneno yaliyo katika maana ya Hip Hop hapo
juu ukitumia mawanda mapana utagundua yana
maana kubwa kama ambavyo yanavyoelezewa
katika aya zinazofuata.
.........itaendelea....

No comments: